USTAWISHAJI VITUNGUU MAJI

 USTAWISHAJI WA VITUNGUU MAJI

USTAWISHAJI WA VITUNGUU MAJI : Zao la vitunguu hulimwa karibu kila mahali hapa nchini. Hata hivyo mikoa ifuatayo hulima vitunguu kwa wingi: Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Iringa, Mara, Mbeya na Dodoma.

Vitunguu na majani yake ni viungo maarufu kwa kuongeza harufu nzuri na ladha katika vyakula. Vile vile hutumika katika kutengeneza supu, siki na kachumbari. Kiafya vitunguu ni muhimu kwani hutupatia madini na vitamini.

 

MAZINGIRA:

Vitunguu huhitaji udongo tifutifu wenye rutuba nyingi na usiotuamisha maji. Hustawi vizuri zaidi kwenye sehemu zenye mwinuko wa kuanzia mita 800 hadi 1,500 kutoka usawa wa bahari. Hupendelea hali, ya ubaridi kiasi wakati wa kuotesha mbegu mpaka vinapoanza kuweka tunguu na joto la wastani (nyuzi joto 20 hadi 27 za Sentgredi) hadi kuvuna. Hivyo ni vizuri vioteshwe wakati wa baridi ili viweze
kuvunwa kipindi cha jua.

 

AINA ZA VITUNGUU:

Aina za vitunguu zinazoshauriwa kustawishwa katika ukanda wa joto ni:- Red Creole, Texas Grano, Tropical Red Fl Hybrid, Red Bombay, ingida Local na Pretoria Grano.

 

KUOTESHA MBEGU KATIKA KITALU

Mbegu za vitunguu huoteshwa kwanza kwenye kitalu na baadaye huhamishiwa shambani. Matayarisho ya kitalu hufanyika wiki moja au mbili kabla ya kupanda mbegu. Tengeneza tuta lenye upana wa mita moja na urefu wowote kutegemea mahitaji yako. Weka mbolea kiasi cha ndoo moja hadi mbili katika kila mita mraba mmoja. Changanya mbolea hii na udongo vizuri. Sawazisha kwa kutumia reki au kifaa chochote.

Mwagilia kitalu siku moja kabla ya kupanda. Sia mbegu katika mistari yenye nafasi ya sentimita 10 hadi 15 kutoka mstari hadi mstari. Kiasi cha mbegu kinachotakiwa kuotesha katika eneo la mita mraba moja ni gramu tano ambacho ni sawa na kijiko kidogo cha chai. Kiasi hiki pia hutoa miche inayotosha kupandikiza eneo la mita mraba 100. Kilo mbili hadi 2½ za mbegu hutoa miche ambayo inatosha kupandikiza katika hekta moja.

Baada ya hapo weka matandazo kama vile nyasi, kisha mwagilia mara mbili kila siku (asubuhi na jioni) hadi mbegu zitakapoota. Mbegu bora huota baada ya siku 10 mpaka 12.

 

KUTAYARISHA SHAMBA

Tayarisha shamba vizuri mwezi mmoja kabla ya kupandikiza. Katua udongo katika kina cha kutosha (sentimita 30). Kisha lainisha udongo wiki mbili kabla ya kupandikiza. Weka mbolea za asili zilizooza vizuri ili kuufanya udongo ushikamane vizuri na uweze kuhifadhi unyevu kwa muda mrefu. Kiasi kinachotosha hekta moja ni tani 20 au zaidi. Changanya mbolea hii na udongo vizuri kisha tengeneza matuta kufuatana na nafasi ya kupandia.

 

KUPANDIKIZA:

Miche inakuwa tayari kwa kupandikizwa shambani baada ya wiki sita tangu kusia mbegu. Wakati huo miche inakuwa na urefu wa sentimita 12 hadi 15 na unene uliosawa na kalamu ya risasi.

Loanisha kitalu siku moja kabla ya kung’oa miche ili kuepuka kukata mizizi. Tumia kijijti au chombo chochote kinachofaa kwa kung’oa. Baada ya kung’oa punguza majani na mizizi ili kuzuia upotevu wa maji.

Pandikiza miche katika nafasi ya sentimita 30 kutoka mstari hadi mstari na sentimita 8 hadi 12 mche hadi mche. Vitunguu vilivyopandwa kwa nafasi hii hukomaa mapema na idadi ya mimea kwa eneo ni kubwa.

Chagua miche yenye afya na ambayo haikushambulia na wadudu wala magonjwa. Miche michanga sana au iliyokomaa sana haifai kwa kupandikiza. Miche ipandikizwe katika kina kama vile ilivyokuwa kwenye kitalu. Pandikiza wakati wa asubuhi au jioni ili kuepuka jua kali na joto linaloweza kuunguza miche. Mara baada ya kupandikiza mwaga maji. Endelea kumwagilia asubuhi na jioni mpaka miche itakaposhika vizuri.

 

KUTUNZA SHAMBA:

KUWEKA MBOLEA:

Mbolea ya kukuzia kama vile CAN au S/A huwekwa shambani katika wiki ya tatu na ya sita baada ya kupandikiza. Weka kiasi cha mifuko mitatu kwa hekta katika wiki ya tatu na mifuko minne katika wiki ya sita. Mbolea iwekwe kwenye mstari na isiguse mimea. Mche mmoja huhitaji kiasi cha kijiko kimoja cha chai na hakikisha udongo una unyevu wa kutosha wakati wa kuweka mbolea.

 

KUMWAGILIA:

Kila wakati hakikisha shamba lina maji ya kutosha. Punguza kumwagilia wakati vitunguu, vinakomaa. Vitunguu vinavyokomaa majani hubadilika rangi kuwa njano. Maji mengi husababisha vitunguu kuoza baada ya kukomaa.

 

PALIZI:

Palilia na tifulia mara kwa mara uonapo magugu yanaota, na hasa miche inapokuwa bado michanga. Palizi ifanyike kwa uangalifu bila kuikata mizizi. Wakati unapopalilia katikati ya mstari ni vema kung’oa magugu kwa mikono na kufunika shina kwa kupandisha udongo kuzuia mizizi isipigwe na jua.

 

MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU:

MAGONJWA

  • UBWJRI VINYONYA (DOWNY MILDEW);

Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hupendelea hali ya unyevunyevu. Dalili zake m majani kuwa na ukungu au uyoga wa rangi ya njano iliyochanganyika na nyeupe. Kwa kawaida majani yaliyoshambuliwa hukauka kabla ya vitunguu kukomaa.

UBWJRI VINYONYA (DOWNY MILDEW)
UBWJRI VINYONYA (DOWNY MILDEW)

Ubwiri vinyoya huzuiwa kwa kuzingatia yafuatayo:

– Kubadilisha mazao. Baada ya kuvuna vitunguu, zao linalofuata lisiwe lajamii moja kama vile vitunguu saumu na liki.

– Nyunyuzia mojawapo ya dawa za kuzuia ukungu kama vile Farmleton, Tebufarm, Funco na Salfarm ambazo hupatikana kwenye Maduka ya FARMERS CENTRE na FARMBASE na wasambazaji wao mikoani.

MADAWA YA KUKABILIANA NA DOWNY MILDEW
MADAWA YA KUKABILIANA NA DOWNY MILDEW

 

  • PURPLE BLOTCH:

Huu pia ni ugonjwa uletwao na ukungu na hushambulia majani, shingo na vitunguu vilivyokomaa. Dalili zake ni, majani huonyesha vidonda vyeupe na vilivyodidimia. Baadaye baka la zambarau huonekana katikati ya jani. Baka hili baadaye huwa jeusi na hufunikwa na uyoga au ukungu. Shina lililoshambuliwa hulegea na huanguka katika wiki ya tatu au ya nne baada ya dalili za ugonjwa huu kuonekana.

PURPLE BLOTCH
PURPLE BLOTCH

Vituguu vilivyokomaa huoza kuanzia shingoni, hugeuka rangi na kuwa njano iliyochanganyika na nyekundu. Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo:-

– Panda vitunguu vilivyothibishwa na wataalam

– Badilisha mazao

– Vuna vitunguu kwa wakati unaotakiwa.

– Epuka kukwaruza au kuchubua vitunguu wakati wa kuvuna.

– Ondoa masalia ya mazao shambani baada ya kuvuna na kuyachoma.

– Panda vitunguu vinavyovumilia mashambulizi ya ugonjwa huu kama vile vitunguu vyekundu.

– Vilevile unaweza kutumia dawa zifuatazo dhidi ya ugonjwa huu Farmleton, Tebufarm, Funco na Salfarm ambazo pia hupatikana kwenye Maduka ya FARMERS CENTRE na FARMBASE na wakala wao mikoani.

MADAWA YA KUKABILIANA NA PURPLE BLOTCH
MADAWA YA KUKABILIANA NA PURPLE BLOTCH

 

  • KUOZA SHINGO (NECKROT):

Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hupendelea sana hali ya unyevu. Hushambulia vitunguu vilivyokwisha vunwa na kuhifadhiwa.

KUOZA SHINGO
KUOZA SHINGO

Vitunguu vilivyoshambuliwa na ugonjwa huu huwa laini, hubonyea na huonekana kama vilivyopikwa. Ugonjwa huanzia kwenye shingo na baadae huenea kwenye kitunguu chote na kufunikwa na ukungu wa kijivu. Mwisho machipukizi madogo dogo hujitokeza. Ugonjwa huu unazuiwa kwa kuzingatia yafuatyo:-

– Vuna vitunguu vilivyokomaa kwa wakati unaotakiwa.

– Badilisha mazao

– Panda vitunguu vilivyothibitishwa na wataalam.

– Ondoa na yachome moto masalia ya mazao baada ya kuvuna.

– Epuka kuchubua au kukwaruza vitunguu wakati wa kuvuna.

– Kausha vitunguu vizuri baada ya kuvuna

– Hifadhi vitunguu kwenye sehemu zisizo na unyevu mwingi au pia waweza kutumia dawa kama Fungicide (eg. Funco), Farmleton, na Superclop

MADAWA YA KUKABILIANA NA UGONJWA WA KUOZA SHINGO
MADAWA YA KUKABILIANA NA UGONJWA WA KUOZA SHINGO

 

WADUDU WAHARIBIFU:

  • SOTA (CUTWORMS):

Hawa ni funza wenye rangi ya kijivu. Hupendelea kujichimbia katika udongo wakati wa mchana, na wakati wa usiku hukata miche michanga karibu na usawa wa ardhi.

Zuia wadudu hawa kwa kutumia majivu au dawa kama vile Fiprofarm na Nogozone mara baada ya kupanda. Kama mche utakatwa, mtoe
mdudu kwa kumfukua na kumwuua, kisha pandikiza mche mwingine.

MADAWA YA KUDHIBITI CUTWORMS
MADAWA YA KUDHIBITI CUTWORMS

Njia nyingine ya kumzuia mdudu huyu ni kuweka shamba na mazingira yake katika hali ya usafi ili wasiweze kuzaliana kwa wingi. Ikiwezekana tifua udongo bila kupanda zao lolote kwa muda wa mwezi mmoja.

 

  • VITHIRIPI (ONION THRIPS):

Ni vidudu vidogo vyenye rangi ya kijivu iliyochanganyika na kikahawia. Mashambulizi hufanywa na funza ambao wana rangi ya njano iliyopauka. Hushambulia majani na kuyasababisha kuwa na michirizi meupe inayong’aa. Mashambulizi yakizidi majani hunyauka na mwishowe mmea hukauka na kufa. Zuia vidudu hivi kwa kutumia dawa kama vile Fiprofarm, Piricarb, Duducron, Darsfarm na Dimefarm

UGONJWA WA VITHIRIPI
UGONJWA WA VITHIRIPI

 

KUVUNA

Vitunguu huwa tayari kwa kuvunwa baada ya miezi mitatu mpaka mitano (siku 90 hadi 150) tangu kusia mbegu, kutegemea aina ya mbegu na hali ya hewa. Anza kuvuna vitunguu uonapo asilimia 50 ya vitunguu vimelegea na kunyauka Ukivuna vitunguu kabla havijakomaa huharibika mapema. Wakati wa kuvuna, ng’oa shina zima na kata majani yajuu na mizizi. Baada ya kuvuna kausha vitunguu vizuri katika sehemu yenye hewa ya kutosha, na ambayo haina unyevu walajua kali.

 

KUHIFADHI:

Kabla ya kuhifadhi vitunguu, hakikisha vimekauka vizuri. Hifadhi vitunguu vilivyokauka vizuri katika sehemu yenye hewa ya kutosha, isiyokuwa na unyevu wala jua kali. Vitunguu visipokauka vizuri vitaoza. Hifadhi vitunguu kwa kutandaza juu ya chanja au funga pamoja mashina yake yaliyokauka na yaning’inize kwenye sehemu ya kuhifadhi ili vitunguu vikauke vizuri.Vitunguu vinaweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi mitatu hadi sita kama hali ya hewa haina unyevu. Aina ya vitunguu vidogo huweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu zaidi kuliko aina kubwa.

 

MAVUNO:

Mavuno hutegemea utunzaji mzuri wa shamba, hali ya hewa na aina ya mbegu. Zao lillotunzwa vizuri huweza kutoa tani 30 hadi 40 kwa hekta.

 

KUBADILISHA MAZAO:

Vitunguu m zao linalotumia chakula kingi ardhini hivyo baaada ya kuvuna lifuatiwe na zao linalotumia chakula kidogo ili kuhifadhi rutuba. Aidha baada ya kuvuna vitunguu, zao linalofuatia lisiwe la jamii moja na vitunguu kama vile vitunguu saumu na iliki ili kuzuia kuenea kwa magonjwa na wadudu wanaoshambulia jamii hii ya mazao.

Post a Comment

Comment what you think about
© KWETU AFYA. All rights reserved. Developed by Jago Desain